Watemi
wa Kisukuma Kanda ya Ziwa Victoria na viongozi wa Chama Cha Watu Wenye
Ualbino nchini Tanzania( Tanzania Albinism Society -TAS) wamefanya usafi
wa mazingira kisha kula chakula cha pamoja na watoto wenye ualbino
wanaolelewa katika kituo cha Buhangija katika manispaa ya Shinyanga.
Watemi
hao wakiongozwa na Katibu Watemi wa Kisukuma Kanda ya Ziwa, Mtemi
Charles Balele Itale wa Bujashi wilaya ya Magu mkoa wa Mwanza
walitembelea kituo hicho leo Jumamosi Julai 8,2017.
Mwenyekiti
wa Chama Cha Watu Wenye Ualbino nchini Tanzania -TAS taifa, Nemes Temba
alisema chama hicho kimekuwa na ushirikiano mkubwa na machifu wa kanda
ya ziwa hicho kuamua kushiriki nao katika kufanya usafi wa mazingira
katika kituo cha Buhangija.
“Malengo
ya kuja hapa kwanza ni kuunga mkono serikali ya awamu ya tano kuhusu
masuala ya usafi,pili ni kuwapa ujumbe watoto hawa kuwa wawe na
utamaduni wa kufanya usafi hata wanaporudi kwenye familia zao,tatu
tumekuja kula chakula cha pamoja na watoto hawa ili kuonesha kuwa tuko
pamoja nao”,alieleza Temba.
Temba
alitumia fursa hiyo kuiomba serikali kuchunguza utitiri wa mashirika
yaliyoanzishwa nchini ambapo sasa yapo zaidi ya 10 na kufuatilia vituo
mbalimbali vilivyoanzishwa kwa lengo la kuwahudumia watu wenye ualbino
hususani watoto kwani sasa vipo takribani 20 lakini wahusika wa vituo
hivyo hawasaidii walengwa.
Temba
alisema mashirika mengi yamekuwa yakijikita katika kupiga vita mauaji
ya watu wenye ualbino huku yakisahau kuwa watu wenye ualbino
wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa elimu na saratani
ya ngozi ambayo imekuwa ikiua watu wengi wenye ualbino.
Katibu
Watemi wa Kisukuma Kanda ya Ziwa, Mtemi Charles Balele Itale wa Bujashi
wilaya ya Magu mkoa wa Mwanza alimpongeza mwenyekiti wa Chama cha Watu
wenye Ualbino kuwakutanisha pamoja katika kituo hicho.
“Juhudi hizi zinaonesha jinsi tunavyowatambua,tunavyowapenda na
tunavyowajali watu wenye ualbino,kwa hiyo katika nafasi zetu za nyadhifa
mbalimbali tunajitahidi kuelimisha na kuwezesha jamii
iwatambue,iwajali,iwapende na kuwapokea katika jamii na watoto warudi
kwenye familia zao na kuishi kama watoto wengine”,alieleza Mtemi
Balele.
“Nimefurahishwa na taarifa ya uongozi wa kituo hiki kuwa sasa watoto
wameanza kwenda likizo kuwaona wazazi wao,hili ni jambo jema sana,Sisi
machifu tuna jukumu letu ni kuielimisha jamii
iwapokee,iwakubali,isiwanyanyase,isiwanyanyapae hivyo sisi kwa
kushirikiana na TAS tutashirikiana katika kutafikia hayo
malengo”,aliongeza Mtemi Balele.
Awali akizungumza katika kituo hicho,Mwalimu Mlezi wa Shule ya Msingi
Buhangija, Frola Kakutebe alisema kati ya watoto wenye ualbino
140,waliopo katika kituo hicho,72 wameenda likizo na 68 wamebakia
kituoni baada ya shule kufungwa kinyume na miaka ya nyuma ambapo watoto
hao walikuwa hawaendi likizo kuonana na ndugu zao.
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo,Selemani Kipanya aliiambia Malunde1 blog
kuwa,sasa Kituo hicho kimepoteza sifa ya kuitwa kituo bali ni shule
kwani tofauti na siku za nyuma hivi sasa watoto wanaoishi hapo wote
wanasoma shule na wanaishi katika mabweni yaliyopo katika shule hiyo.
ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI
Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527
0 تعليقات