JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limesema nia ya kuongeza uandikishaji wa vijana wenye elimu ya juu jeshini unalenga kuwa na askari wenye uwezo mkubwa wa kutafsiri mambo haraka.
Hayo yalielezwa na Mkuu wa Chuo cha Kijeshi cha Uongozi Monduli (TMA), Meja Generali Paul Masao alipokuwa akifunga mafunzo ya askari 1,833.
Kundi hilo la 37 la Mwaka 2016 lilipikwa kwa Wiki 18 katika Shule ya Mafunzo ya awali ya kijeshi (RTS Kihangaiko) mkoani Pwani, kisha kufunga mafunzo yao Uwanja wa Jeshi la Kujenga Taifa Oljoro 833KJ.
Akizungumza baada ya gwaride la mwendo wa pole na haraka kutoa heshima, maonyesho ya askari waliohitimu na kula kiapo cha utii Meja Generali Masao aliwataka wahitimu hao kuitumia elimu ya juu kama chachu ndani ya JWTZ.
“Nia ya JWTZ kuongeza uandikishaji wa askari wenye elimu ya juu ni
kuwezesha uwapo wa askari wenye elimu ya kuwawezesha kutafsiri
mambo haraka,” alisema Meja Generali Masao na kuongeza:
“Elimu mliy
onayo ikawe chachu ndani ya jeshi,ikalete matokeo chanya kazini.Isibakie kuandikisha wasomi wasiokuwa na matunda.Tunataka kuona elimu ikisaidia kufungua wigo wa uelewa
kwa wanajeshi wetu,” alisema.
Aidha aliwataka askari hao kujiepusha na matumizi ya nguvu migogoro kati yao na raia, ikiwamo marufuku kujihusisha na vikundi vya dawa za kulevya, bangi, unyanyasaji na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.
“Itumieni kwa busara mitandao ya kijamii si kwamba hatutaki
muitumie lakini wanajeshi siku zote tuna akiba ya maneno kwani tunaongozwa na miiko yetu.
“Tukikubaini dhidi ya vitendo hivi utakuwa umepoteza sifa jeshini na
utafukuzwa. Niwasihi jiendelezeni kielimu fanyeni mambo ya
kimaendeleo ili kuepuka kudhalilika wakati wa kustaafu,” alisema
Meja Generali Masao alitumia fursa hiyo pia kuwakumbusha askari hao jukumu lililombele yao la kulinda nchi dhidi ya maadui wa ndani na nje, ikiwamo kusaidia majanga ya kitaifa na kimataifa watakapohitajika.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Mafunzo ya awali ya Kijeshi, RTS Kihangaiko Kanali Chilo Okombo alisema kuwa askari hao 1,833 wamefanya vizuri katika masomo yao huku askari 6 wakishindwa kuhitimu kutokana na sababu mbalimbali.
Naye Kamanda Kikosi cha 833 KJ Oljoro Luteni Kanali Sijaona Myala aliwataka wahitimu hao kuhakikisha wanazingatia mambo ya msingi ambayo ni utii, uhodari na kuheshimu sheria.
Mbali ya kuhudhuriwa na maofisa mbalimbali wa jeshi sherehe hizo zilihudhuriwa pia na wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini waliofika kushuhudia ndugu na jamaa zao wakihitimisha mafunzo ya awali ya kijeshi.
0 تعليقات